Mnamo tarehe 8 Aprili, wapiga kura wa Kansas City wataombwa kuongeza muda wa kodi ya mauzo ya usalama wa jamii kwa miaka 20 kwa gharama ya dola milioni 484. Kwa kawaida, kodi hii imefadhili huduma muhimu kama vile wapokea simu za dharura za 911 na watoa huduma za dharura. Hata hivyo, safari hii, angalau dola milioni 250 zitafadhili ujenzi wa gereza la jiji, huku dola milioni 375 za ziada zikihitajika kwa ajili ya wafanyakazi na matengenezo ya kituo hicho. Hiyo ni zaidi ya dola nusu bilioni za walipa kodi zinazotumika kwenye gereza ambalo halingetatua mahitaji yetu ya usalama wa jamii.
Mara kwa mara nasikia kutoka kwa majirani zangu kote Kansas City kuhusu wasiwasi wao juu ya usalama wa jamii. Hadithi kuhusu mauaji, wizi wa magari kwa nguvu, uvunjaji wa nyumba wa mfululizo na vurugu za bunduki zinazoendelea ni za kawaida. Lakini gereza la jiji halitatatua masuala haya kwa sababu makosa kama vile mauaji, wizi mkubwa wa gari, wizi au uharibifu wa mali wa zaidi ya dola 750 ni makosa ya jimbo ambayo yangeshughulikiwa katika ngazi ya kaunti. Walipa kodi tayari wanatumia dola milioni 301 kwa gharama za ujenzi wa gereza jipya la Kaunti ya Jackson.
Kama mjumbe wa Halmashauri ya Jiji wa Wilaya ya 6, nilihudumu katika Kamati ya Jiji ya Kizuizini na Urekebishaji Tabia (Municipal Detention and Rehabilitation Committee) ili kupitia kwa karibu zaidi uhitaji wa jiji wa kuwa na gereza jipya. Watu wengi wanaoingia katika mfumo wa gereza la jiji letu wanashikiliwa kwa makosa madogo — kukojoa hadharani, kulala nje, kuingia kwenye eneo la mtu bila ruhusa au wizi mdogo — na mara nyingi hawana makazi au wanakabiliwa na ugonjwa wa akili ambao haujatibiwa. Wengi wanabaki gerezani kwa sababu hawana uwezo wa kiakili wa kusimama mahakamani au kwa sababu tu hawawezi kulipia dhamana.
Jaji wa Mahakama ya Jiji Martina Peterson alieleza hivi karibuni kwa KSHB, “Nataka waachiwe huru, lakini bado hawajatengemaa kiasi cha kuachiwa huru kwa sababu bado wanasikia sauti.”
“Baadhi ya watu hawa wanapaswa kuwa katika hospitali ya afya ya akili badala ya kituo cha kizuizini wakati wanapopitia mfumo wa mahakama ya jiji,” mjumbe wa Halmashauri ya Jiji Crispin Rea, mtetezi mwingine wa kodi ya gereza, alieleza kwa Martin City Telegraph.
Gereza jipya la jiji halitatatua matatizo haya — litayakusanya tu mahali pamoja. Wasio na makazi wanabaki bila nyumba na mahitaji ya afya ya akili hayatimizwi. Kwa kifupi: Gereza jipya la jiji ni suluhisho lingine la muda na la gharama kubwa ambalo lingeendelea kuwaingiza na kuwatoa gerezani watu walio katika hali ngumu.
Kansas City haipaswi kuwa katika biashara ya kuwafunga gerezani wale ambao kosa lao kubwa zaidi ni kuhitaji msaada wa kitaalamu wa afya ya akili. Njia hii ni ghali na haina utu, na haifanyi chochote kuzuia uhalifu na kuboresha matokeo yetu ya usalama wa jamii.
Nini kilitokea kwa upande wa “urekebishaji tabia” wa kituo cha urekebishaji tabia na kizuizini?
Mwaka wa 2019, washauri walipendekeza kituo cha rasilimali za jamii ili kusaidia wafungwa wanaoingia na kutoka gereza, kuboresha matokeo na kupunguza kurudia uhalifu. Hata hivyo, kama sehemu ya makubaliano ya dola milioni 2.3 ya jiji kununua ardhi kutoka kaunti, makubaliano hayo yanazuia wafungwa kuachiliwa katika eneo hilo, jambo ambalo kwa vitendo linakataza kituo hicho kujengwa pamoja na gereza. Zaidi ya hayo, kodi hii haijumuishi ufadhili wa CRC au kitu chochote kama hicho.
Suluhisho la kweli la kupunguza kurudia uhalifu, usalama wa jamii
Tangu Oktoba 2024, nimekuwa nikifanya kazi na wenzangu pamoja na mahakama ya jiji kuhusu pendekezo la kituo cha rasilimali za jamii ambacho kingeboresha matokeo kwa wafungwa wetu, kupunguza kurudia uhalifu na kuboresha usalama wa jamii.
CRC hii ingefuata mfano wa Criminal Mental Health Project kutoka Kaunti ya Miami-Dade, Florida, ambao umepunguza kiwango cha kurudia uhalifu kutoka 76% hadi 20%. Kituo hiki kingeweka rasilimali za mahakama sehemu moja na kingejumuisha kituo cha kuondoa uraibu mwilini, makazi ya muda na wasaidizi wa huduma ili kuwasaidia watu kupata nyumba, bima ya afya, huduma ya afya ya akili na ajira. Suluhisho kama hizi hupunguza utegemezi wetu wa magereza na hivyo kupunguza gharama zetu za gereza, lakini kodi hii ya gereza haitafadhili CRC.
Kwa sasa hakuna mpango katika kodi ya mauzo inayopendekezwa wa kujumuisha au kufadhili urekebishaji tabia. Bila urekebishaji tabia, wafungwa wetu wataendelea kuzungushwa kupitia mahakama zetu na mfumo wa gereza, na kuwagharimu walipa kodi mamilioni ya dola kwa mwaka bila kushughulikia sababu iliyowafanya wawe kwenye gereza tangu mwanzo.
Njia mbadala za gereza huboresha matokeo na kupunguza uhitaji wetu wa gereza, jambo linalookoa pesa za walipa kodi huku likiongeza usalama wa jamii.
Tunajua kuwa rasilimali za jamii huokoa pesa na maisha huku zikiongeza usalama wa jamii — lakini, mwaka baada ya mwaka, Kansas City inatenga fedha nyingi zaidi kwa usimamizi wa sheria kuliko nyumba, afya ya umma na msaada kwa watu wasio na makazi. Kwa kila dola 1 tunayotumia kwa afya ya umma, tunatumia dola 12 kwa usimamizi wa sheria; kwa kila dola 1 tunayotumia kwa nyumba, tunatumia dola 12 kwa usimamizi wa sheria; kwa kila dola 1 tunayotumia kwa tatizo la ukosefu wa makazi, tunatumia dola 74 kwa usimamizi wa sheria. Kila mwaka, matumizi kwenye usimamizi wa sheria yanapoongezeka, ndivyo uhalifu unavyoongezeka pia.
Viongozi wa Kansas City wameshindwa kuzisaidia jamii zetu zinazoathirika zaidi na uhalifu kwa sababu tunapendelea kufanya kile kinachofaa zaidi kisiasa badala ya kile kinachohitajika ili kuboresha matokeo kwa watu wetu. Tumetoa fedha chache kwa rasilimali muhimu kama vile nyumba za bei nafuu, huduma za afya ya akili na shule, tukipa kipaumbele utekelezaji wa sheria badala yake. Gereza jipya linapaswa kuwa chaguo la mwisho, lakini kodi hii inalifadhili kwanza, na kutengeneza mzigo wa kodi wa gharama kubwa na usio wa lazima kwa wakazi wetu huku ikiziacha nyuma suluhisho muhimu za kuwarekebisha tabia ambazo zina rekodi iliyothibitishwa ya kuboresha usalama wa jamii.
Jiunge nami na upige kura ya hapana kuhusu kodi ya gereza, na upige kura ya ndiyo kuhusu dhamana ya shule ili kufadhili shule zetu na kuwekeza kwa watoto wetu tarehe 8 Aprili.
Johnathan Duncan anawakilisha Wilaya ya 6 ya Halmashauri ya Jiji la Kansas City.

